Biblia Todo Logo
Bìoball air-loidhne

- Sanasan -

Hesabu 22 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002


Balamu anaitwa na mufalme wa Moabu

1 Waisraeli wakaanza safari tena, wakaenda kupiga kambi yao katika bonde za Moabu, upande wa mashariki wa muto Yordani, kuelekea muji wa Yeriko.

2 Mufalme Balaki mwana wa Sipori, alijua mambo yote Waisraeli waliyowatendea Waamori.

3 Yeye pamoja na Wamoabu wakashikwa na hofu kubwa juu ya Waisraeli. Waliwaogopa hasa kwa sababu ya wingi wao.

4 Basi Wamoabu wakawaambia viongozi wa Midiani: Makundi haya ya watu sasa hivi yataharibu kila kitu kandokando yetu kama vile ngombe dume anavyokula majani katika shamba. Kwa hiyo, Balaki mwana wa Sipori aliyekuwa mufalme wa Moabu wakati ule,

5 akapeleka ujumbe kwa Balamu mwana wa Beori, huko Petori, karibu na muto Furati katika inchi ya Amawi. Akamwambia Balamu hivi: Kuna taifa ambalo limetoka Misri, nalo limeenea kila pahali katika inchi, tena linatishia kutwaa inchi yangu.

6 Kuja sasa uwalaani watu hawa kwa ajili yangu maana wana nguvu kuliko mimi. Labda nitaweza kuwashinda na kuwafukuza wasiingie katika inchi yangu, kwa maana unajua kwamba wewe ukimubariki mutu anabarikiwa, ukimulaani mutu analaaniwa.

7 Basi, wazee wa Moabu na Midiani wakapeleka zawadi za uaguzi, wakaondoka kwenda kwa Balamu. Walifika, wakamupa Balamu ujumbe wa Balaki.

8 Balamu akawaambia: Mulale huku usiku huu, nami nitawajulisha vile Yawe atakayoniambia. Basi, wazee hao wa Moabu wakakaa na Balamu.

9 Kisha Mungu alimufikia Balamu, akamwuliza: Ni nani hawa wanaokaa nawe?

10 Balamu akamujibu Mungu: Balaki mwana wa Sipori amenitumia ujumbe kwamba

11 kuna watu wa taifa fulani waliotoka Misri, nao wameenea kila pahali katika inchi. Ameniomba niende kuwalaani watu hao kusudi pengine ataweza kupigana nao na kuwafukuza.

12 Mungu akamwambia Balamu: Usiende pamoja na watu hawa, wala usiwalaani watu hao maana wamebarikiwa.

13 Basi, asubui yake Balamu akaamuka, akawaambia wazee wa Balaki: Murudie katika inchi yenu, kwa maana Yawe hapendi kuniruhusu kwenda pamoja nanyi.

14 Kwa hiyo wazee wa Moabu wakaondoka, wakarudi kwa Balaki, wakamwambia: Balamu amekataa kuja pamoja nasi.

15 Kisha, Balaki akatuma wakubwa wengine, wengi zaidi na wa vyeo vya juu kuliko wale wa kwanza.

16 Hao wakafika kwa Balamu, wakamwambia: Balaki mwana wa Sipori anasema hivi: Usikubali kuzuiwa na chochote hata uache kuja kwangu.

17 Nitakupatia heshima kubwa, na chochote utakachoniomba nitakutimizia. Kuja uwalaani watu hawa.

18 Lakini Balamu akawajibu watumishi wa Balaki: Hata kama Balaki atanipa nyumba yake imejaa feza na zahabu, mimi sitaweza kuvunja amri ya Yawe, Mungu wangu, juu ya jambo lolote, dogo au kubwa.

19 Lakini tafazali mulale hapa usiku huu kama wale wenzenu, nami nipate kujua kile Yawe atakachoniambia tena.

20 Basi, Mungu akamufikia Balamu usiku ule, akamwambia: Kama watu hawa wamekuja kukuita, kwenda pamoja nao, lakini fanya tu kile nitakachokuambia.

21 Balamu akaamuka asubui, akatandika punda wake, akaenda pamoja na hao wakubwa.


Balamu, punda na malaika

22 Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu Balamu alikuwa anakwenda; hivyo malaika wa Yawe akakutana naye katika njia. Wakati huo Balamu alikuwa amepanda juu ya punda wake naye alisindikizwa na watumishi wake wawili.

23 Basi, punda akamwona malaika huyo wa Yawe amesimama katika njia, akishika upanga uliochomolewa. Kwa hiyo akaacha njia, akaenda pembeni. Balamu akamupiga huyo punda, akamurudisha katika njia.

24 Kisha malaika huyo wa Yawe akatangulia mbele, akasimama pahali hiyo njia ilikuwa nyembamba, kati ya mashamba ya mizabibu na kuta pande zote mbili.

25 Punda alipomwona malaika huyo wa Yawe, akajibanisha kwenye ukuta na kubana muguu wa Balamu hapo. Kwa hiyo Balamu akamupiga tena huyo punda.

26 Kisha malaika akatangulia tena, akasimama pahali pembamba pasipo na nafasi ya kupita kuume wala kushoto.

27 Punda alipomwona huyo malaika wa Yawe, akalala chini. Balamu akawaka hasira, akamupiga kwa fimbo yake.

28 Hapo Yawe akafungua kinywa cha huyo punda, akamwambia Balamu: Nimekutendea nini hata ukanipiga mara hizi tatu?

29 Balamu akamwambia punda: Wewe umenichekelea! Kama ningekuwa na upanga ningalikuua sasa hivi!

30 Punda akamwambia Balamu: Mimi si yuleyule punda wako aliyekubeba maisha yako yote mpaka siku hii ya leo? Nimekwisha kukutendea namna hii? Balamu akajibu: Hapana.

31 Hapo, Yawe akafungua macho ya Balamu, naye akamwona malaika wa Yawe amesimama katika njia, akishika upanga uliochomolewa toka kifuko chake. Balamu akajitupa uso mpaka chini.

32 Malaika wa Yawe akamwambia Balamu: Mbona umemupiga punda wako mara tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya.

33 Punda wako ameniona akaniepuka mara tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha muzima punda huyu.

34 Balamu akamwambia malaika wa Yawe: Nimetenda zambi maana sikujua kwamba umesimama katika njia kwa kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi kwangu.

35 Lakini malaika wa Yawe akamwambia Balamu: Kwenda na watu hawa, lakini utasema tu kile nitakachokuambia. Basi, Balamu akaendelea na safari pamoja na viongozi wa Balaki.

36 Balaki alipopata habari kwamba Balamu anakuja, akatoka kwenda kumupokea katika muji wa Ari, muji uliokuwa kwenye ukingo wa muto Arnoni kwenye mupaka wa Moabu.

37 Balaki akamwambia Balamu: Kwa nini haukukuja kwangu mara moja nilipokuita? Ulifikiri sitaweza kukupatia heshima ya kutosha?

38 Balamu akamujibu Balaki: Sasa nimekuja! Lakini, nina mamlaka ya kusema neno lolote? Jambo Mungu atakaloniambia ndilo ninalopaswa kusema.

39 Basi, Balamu akaenda pamoja na Balaki. Wakafika katika muji Kiriati-husoti.

40 Huko Balaki akatoa sadaka ya ngombe na kondoo, akawagawanyia Balamu na wakubwa waliokuwa pamoja naye nyama.


Balamu anawabariki Waisraeli

41 Kesho yake, Balaki akamutwaa Balamu, akapanda naye mpaka Bamoti-Bali; kutoka huko, Balamu aliweza kuwaona wamoja kati ya Waisraeli.

Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.

Bible Society of the Democratic Republic of Congo
Lean sinn:



Sanasan