2 Samweli 22 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Wimbo wa ushindi wa Daudi 1 Daudi alimwimbia Yawe wimbo huu siku ile Yawe alipomukomboa toka katika mikono wa waadui zake, na toka katika mukono wa Saulo. 2 Alisema: Yawe ni: kikingio changu, kimbilio langu, mukombozi wangu, 3 Mungu wangu, yule ambaye ninamukimbilia, ngao yangu, nguvu ya wokovu wangu, munara wangu, kimbilio langu. Mwokozi wangu, unaniokoa kutoka watesaji wakali! 4 Ninamwita Yawe anayestahili sifa anisaidie, nami ninaokolewa kutoka kwa waadui zangu. 5 Mawimbi ya kifo yalinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinishambulia, 6 kamba za kuzimu zilinizunguka, mitego ya kifo ilikuwa mbele yangu. 7 Katika taabu yangu, nilimwita Yawe; nilimwita Mungu wangu. Toka katika hekalu lake alisikia sauti yangu; kilio changu kilifika katika masikio yake. 8 Halafu, dunia ikatetemeka na kutikisika, misingi ya mbinguni ikayumbayumba na kuruka, kwa maana Mungu alikuwa amekasirika. 9 Moshi ulifuka kutoka katika pua yake, moto wenye kuteketeza ukatoka katika kinywa chake, makaa ya moto yakatokea. 10 Aliinamisha anga, akashuka chini, na wingu jeusi lilikuwa chini ya miguu yake. 11 Alipanda juu ya kerubi na kuruka; akaruka juu ya mabawa ya upepo. 12 Alijifunika giza pande zote; kifuniko chake kilikuwa mawingu mazito ya mvua. 13 Umeme ulimetameta mbele yake, makaa ya moto yakawaka. 14 Yawe alinguruma kutoka mbinguni; Mungu Mukubwa akatoa sauti yake. 15 Aliwapiga waadui mishale, akawatawanya; alirusha umeme, akawakimbiza. 16 Yawe alipovikaripia, pumzi ya pua yake ilifunua vilindi vya bahari na misingi ya dunia ikaonekana. 17 Mungu alinyoosha mukono wake kutoka juu, akanitwaa, alininyanyua kutoka ndani ya maji mengi. 18 Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu, kutoka hao walionichukia na kuwa na nguvu kunishinda. 19 Walinishambulia nilipokuwa katika taabu, lakini Yawe alinikinga. 20 Alinileta, akaniweka kwenye nafasi ya usalama; aliniponyesha kwa sababu alipendezwa nami. 21 Yawe alinitendea kwa kadiri ya haki yangu; alinilipa kwa vile mikono yangu haina kosa. 22 Maana nimefuata njia za Yawe, wala sikujitenga na Mungu wangu kwa ajili ya uovu. 23 Nimeshika maagizo yake yote, sikuacha kufuata masharti yake. 24 Mbele yake nilikuwa mukamilifu, nimejikinga nisikuwe na kosa. 25 Yawe amenilipa kwa kadiri ya haki yangu, kwa kadiri ya usafi wangu mbele yake. 26 Wewe ni mwema kwa wema, mukamilifu kwa wakamilifu, 27 bila kosa kwa wale ambao hawafanyi makosa, lakini mukali kwa waovu. 28 Wewe unawaokoa wanyenyekevu, lakini unaangalia wenye majivuno kusudi uwashushe. 29 Ee Yawe, wewe ni taa yangu. Yawe anafanya giza langu likuwe mwangaza. 30 Kwa musaada wako, ninashinda kundi la waaskari; kwa musaada wa Mungu wangu, ninaruka kuta. 31 Matendo ya Mungu ni makamilifu. Ahadi ya Yawe ni ya kuaminika. Yeye ni ngao kwa wote wanaomukimbilia. 32 Nani anayekuwa Mungu isipokuwa Yawe? Nani anayekuwa kikingio isipokuwa Mungu wetu? 33 Ni Mungu ambaye ananipatia nguvu, na anaifanya salama njia yangu. 34 Ameiimarisha miguu yangu kama ya swala, na kunilinda salama juu ya milima. 35 Ananifundisha kupigana vita, mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba. 36 Umenipa ngao yako ya kuniokoa; umenifanikisha kwa wema wako. 37 Umepanua njia yangu wala miguu yangu haikuteleza. 38 Niliwafuata waadui zangu na kuwaangamiza; sikurudi nyuma mpaka wamemalizika. 39 Niliwamaliza kabisa. Hawakuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. 40 Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita; uliwaporomosha waadui chini yangu. 41 Uliwakimbiza waadui zangu, na wale walionichukia niliwaangamiza. 42 Walitafuta musaada, lakini hakukukuwa wa kuwasaidia; walimulilia Yawe, lakini hakuwajibu. 43 Niliwatwanga, wakakuwa kama mavumbi, nikawaponda na kuwakanyaga kama matope katika barabara. 44 Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu, ukanichunga kuwa mutawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. 45 Wageni walinifikia wakinyenyekea; waliposikia tu habari zangu, walinitii. 46 Wageni walivunjika moyo; wakakuja kutoka makimbilio yao wakitetemeka. 47 Yawe anaishi! Asifiwe yeye kikingio changu! Atukuzwe Mungu, kikingio na mwokozi wangu. 48 Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi, ameweka mataifa chini yangu. 49 Ameniokoa kutoka waadui zangu. Ee Yawe, ulinitukuza juu ya wapinzani wangu na kuniponyesha kutoka watesaji wakali. 50 Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa; nitaliimbia sifa jina lako. 51 Mungu anamujalia mufalme wake ushindi mukubwa; anamutendea mema muchaguliwa wake, ndiye Daudi na wazao wake milele. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo