Biblia Todo Logo
Bìoball air-loidhne

- Sanasan -

1 Samweli 3 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002


Yawe anamutokea Samweli

1 Wakati huo, kijana Samweli alipokuwa anamutumikia Yawe chini ya uangalizi wa Eli, ujumbe kutoka kwa Yawe ulikuwa mara haba tu; hata na maono kutoka kwake yalipatikana mara chache.

2 Siku moja usiku, Eli ambaye macho yake yalikuwa yamefifia, alikuwa amelala katika chumba chake.

3 Samweli naye alikuwa amelala ndani ya hekalu la Yawe karibu na Sanduku la Agano la Mungu. Taa ya Yawe ilikuwa ingali inawaka maana kulikuwa hakujapambazuka.

4 Halafu Yawe akamwita Samweli, naye Samweli, akaitika: “Niko hapa!”

5 Kisha Samweli akamwendea Eli kwa haraka, akamwambia: “Nimekuja, maana umeniita.” Lakini Eli akamwambia: “Mimi sikukuita. Kwenda ulale.” Samweli akarudi na kulala.

6 Yawe akamwita tena: “Samweli!” Samweli akaamuka, akamwendea Eli na kumwambia: “Nimekuja, maana umeniita.” Lakini Eli akamwambia: “Sikukuita mwana wangu, ulale tena.”

7 Samweli alikuwa hamujui Yawe bado, wala ujumbe wa Yawe ulikuwa bado haujafunuliwa kwake.

8 Yawe akamwita Samweli kwa mara ya tatu. Samweli akaamuka, akamwendea Eli na kumwambia: “Nimekuja, maana umeniita.” Halafu Eli alitambua kwamba Yawe ndiye aliyemwita Samweli.

9 Kwa hiyo Eli akamwambia Samweli: “Kwenda ulale, na akikuita, umwambie hivi: ‘Sema, ee Yawe, maana mimi mutumishi wako ninasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akarudi na kulala pahali pake.

10 Kisha Yawe akakuja na kusimama hapo, akamwita Samweli kama pale mbele: “Samweli! Samweli!” Samweli akasema: “Sema, maana mimi mutumishi wako ninasikiliza.”

11 Kisha, Yawe akamwambia Samweli: “Ninataka kutenda jambo fulani katika Israeli ambalo kila mutu atakayesikia, atashituka kwa kulisikia.

12 Siku hiyo, nitatimiza yale yote niliyosema tangu mwanzo mpaka mwisho juu ya Eli na juu ya jamaa yake.

13 Nimekwisha kumwambia kwamba nitaiazibu jamaa yake milele, kwa uovu anaoujua kwa sababu wana wake wamenikufuru mimi na hakuwazuia.

14 Kwa hiyo ninaapa juu ya jamaa ya Eli kwamba uovu wao hautaondolewa hata kidogo kwa matoleo wala kwa sadaka.”

15 Samweli akalala pale mpaka asubui, kisha akaamuka na kufungua milango ya nyumba ya Yawe. Lakini Samweli aliogopa kumwambia Eli maono hayo.

16 Hata hivyo, Eli alimwita Samweli, akamwambia: “Mwana wangu Samweli.” Samweli akaitika: “Niko hapa!”

17 Eli akamwuliza: “Yawe alikuambia nini? Usinifiche alichokuambia. Ikiwa utanificha kitu alichokuambia, Mungu akuazibu vikali.”

18 Basi, Samweli akamwelezea Eli yote aliyoambiwa, bila kumuficha chochote. Halafu Eli akasema: “Yeye ni Yawe; afanye anachoona ni chema kwake.”

19 Samweli aliendelea kukomaa na Yawe akakuwa pamoja naye, na yale yote aliyosema hakuna hata moja ambalo halikutimia.

20 Watu wote katika inchi ya Israeli toka Dani, upande wa kaskazini, mpaka Beri-Seba, upande wa kusini, wakajua kwamba Samweli alikuwa nabii mwaminifu wa Yawe.

21 Yawe alizidi kujionyesha kule Shilo, ambako alimutokea Samweli na kuongea naye. Naye Samweli aliposema kitu, Waisraeli wote walimusikiliza.

Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.

Bible Society of the Democratic Republic of Congo
Lean sinn:



Sanasan