1 Mambo ya Siku 14 - BIBLIA Maandiko Matakatifu Kwa Watu Wote 2002Kazi za Daudi katika Yerusalema ( 2 Sam 5.11-16 ) 1 Kisha mufalme Hiramu wa Tiro akatuma wajumbe kwa Daudi, akamupelekea vilevile miti ya mierezi, wajengaji na waseremala, kusudi wamujengee Daudi nyumba ya kifalme. 2 Halafu, Daudi akatambua kwamba Yawe amemwimarisha akuwe mufalme wa Israeli, na kwamba ufalme wake umetukuzwa kwa ajili ya Waisraeli, watu wake. 3 Kule Yerusalema, Daudi akaoa wake wengi zaidi, naye alizaa wana na wabinti wengine. 4 Haya ndiyo majina ya watoto aliozaa kule Yerusalema: Samua, Sobabu, Natani, Solomono, 5 Ibuhari, Elisua, Elipeleti, 6 Noga, Nefegi, Yafia, 7 Elisama, Beliada na Elifeleti. Daudi anawashinda Wafilistini ( 2 Sam 5.17-25 ) 8 Wafilistini waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mufalme wa inchi nzima ya Waisraeli, wote wakatoka kwa wingi kwenda kumutafuta. Daudi alipopata habari, akatoka kwenda kupigana nao. 9 Wafilistini wakafika wakaanza mashambulizi katika bonde la Refaimu. 10 Halafu Daudi akamwomba Mungu shauri: “Niende kuwashambulia Wafilistini? Utawatia katika mikono yangu?” Naye Yawe akamwambia: “Kwenda, nitawatia katika mikono yako.” 11 Basi, Daudi akaenda kule Bali-Perasimu, akawashinda; halafu akasema: “Mungu amebomoa ukingo wa waadui zangu kwa mukono wangu, kama mafuriko ya maji yanayoenda mbio.” Kwa hiyo pahali pale panaitwa “Bwana Mwenye Kubomoa.” 12 Wafilistini walipokimbia, waliacha sanamu za miungu yao kule, naye Daudi akatoa amri zote zichomwe kwa moto. 13 Kisha Wafilistini wakafanya mashambulizi katika bonde lile kwa mara ya pili. 14 Mara hii, Daudi alipoomba shauri kwa Mungu, Mungu akamwambia: “Usiwashambulie kutokea hapa, lakini zunguka nyuma yao na kuwashambulia kutokea mbele ya miti ya miforosadi, halafu uwashambulie kutokea kule. 15 Na mara moja utakaposikia vishindo vya miguu kwenye vilele vya ile miforosadi, halafu, toka uende katika vita. Nitakuwa nimekwisha kukutangulia kuwapiga waaskari wa Wafilistini.” 16 Daudi akafanya kama vile alivyoamuriwa na Mungu. Akawapiga waaskari wa Wafilistini kutokea Gibeoni mpaka Gezeri. 17 Daudi akakuwa na sifa popote katika inchi, naye Yawe akayatia hofu mataifa yote, nayo yakamwogopa sana. |
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.
Bible Society of the Democratic Republic of Congo